Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, linawashikilia watu saba kwa matukio mbalimbali ya uhalifu, wakiwamo vijana watano wanaodaiwa kuhusika na mauaji ya mlinzi wa SUMA-JKT. Wanadaiwa kumkata mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake kisha kumpora bunduki na kutokomea nayo. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Mohammed Mpinga, alisema Februari 26, mwaka huu ya saa 1:30 jioni, vijana hao wakiwa na mapanga, walimvamia na kumshambulia mlinzi huyo, Chewe Wilson (34), akilinda kituo cha mafuta cha Manyanya kilichopo Uyole. Aliwataja vijana hao ni Hamis Shaban (19) na Ibrahim Mbilinyi (22) wote wakazi wa Itezi, Stan Wema (21) mkazi wa Uyole, Bahati Laulend (22) mkazi wa Iduda na Sambaa Samson (32) mkazi wa Isyeseye. Alisema vijana hao baada ya kumjeruhi wakidhani amekufa walimpora bunduki aina ya Shortgun, mali ya SUMA-JKT aliyokuwa anaitumia na kutokomea nayo. Hata hivyo, alisema mlinzi huyo alikutwa na wasamaria wema akiwa hai na kukimbizwa katika Hospitali ya Kanda ya ...