Serikali ya Tanzania yatishia kuufunga mgodi wa Acacia Tarime
Waziri wa Madini Doto Biteko ametishia kuufunga mgodi wa ACACIA North Mara ifikapo Machi 30 mwaka huu, endapo utashindwa kudhibiti maji yenye sumu kwenda kwenye makazi ya watu.
Waziri Biteko ameyasema hayo baada kushuhudia kiasi kikubwa cha maji hayo yakielekezwa kwenda maeneo ya wananchi.
- Tshisekedi na Kabila watangaza serikali ya Muungano
- R Kelly avunja ukimya
- Je Mbowe na Matiko wataachiliwa leo?
- Je, siri za watumiaji wa Facebook zitalindwa kweli?
Akizungumza baada ya kukagua miundo mbinu ya maji machafu katika mgodi huo, siku ya Jumanne, waziri huyo ameutaka mgodi huo kuhakikisha tatizo la maji linapatiwa ufumbuzi kabla ya tarehe 30 mwezi Machi.
''Serikali haitajali muwekezaji, sisi maisha ya Mtanzania hata mmoja ni muhimu mno, nyie kwa kuwa mnafanya biashara, mnatakiwa kuzingatia usalama wa watu hapa'' Alisisitiza waziri Biteko.
Kwa mujibu wa waziri Biteko, tayari serikali imekwishatuma timu ya wataalamu kukagua mgodi huo, na kwamba wamekwishapewa muongozo juu ya ni nini cha kufanya kulingana na sheria na taratibu.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezwaji wa agizo la rais wa Tanzania John Pombe Magufuli alilolitoa Septemba mwaka jana, ambaye aliwataka wahusika kutatua matatizo yanayowakabili wakazi wanaoishi maeneo ya mgodini, likiwemo suala la maji ya sumu.
Mbunge wa Tarime vijijini John Heche alitaka malipo na fidia ilipwe kwa wakati wa maeneo ya mgodi wa ACACIA walioathiriwa na sumu: '' kwasababu maji ya sumu wote tumekiri kuwa yale maji yalikuwa yanachuruzika kutokana na uzembe wa watu wamefanyiwa tathmini ya malipo tangu mwaka 2014 walipwe fidia zao'', alisisitiza Bwan Heche.
Maji ya sumu yanayotiririka kutoka kwenye mgodi wa ACACIA yamekuwa kero kwa wanavijiji wanaoishi karibu nao kutokana na kuwasababishia matatizo ya kiafya miongoni mwake yakiwa ni magonjwa ya ngozi.
Mapema wiki hii Kaimu mkuu wa mgodi wa Uchimbaji wa Dhahabu ACACIA North Mara Nyamongo Wilayani Tarime John Omongi alisema: ''mgodi unatarajia kuwalipa fidia ya zaidi ya Shilingi Bilioni 3.8 ardhi kwa wananchi ambao majina yao yamekwisha fikishwa kwenye serikali za vijiji vya Nyabichune,Mjini Kati,Nyangoto na Nyakunguru''.
Awali rais Magufuli aliwataka wakuu wa wilaya na wakuu wa mikoa nchi nzima kushughulikia katika Mji wa Nyamongo ili wananchi kulipwa fidia na Mgodi wa Acacia North Mara.
Si mara ya kwanza kwa wachimbaji wa mgodi wa madini wa Acacia kujipata mashakani
Serikali imekuwa ikiituhumu kampuni hiyo kwa kukwepa kodi, udanganyifu na kusafirisha mchanga wenye madini nje ya nchi kinyume na sheria.
Mapema mwezi Januari mwaka huu , kampuni hiyo ya Acacia Mining ilitozwa faini ya Sh300 ($130,000) kwa tuhuma za uchafuzi wa mazingira katika mgodi wake wa North Mara.
Acacia ilikanusha madai hayo wakidai kila wakifanyacho ni kwa mujibu wa sheria za Tanzania na mikataba ya ndani na ya kimataifa waliyoafikiana.
Acacia na serikali ya Tanzania wamekuwa kwenye mahusiano magumu toka mwaka 2017.
Mwaka 2017 serikali ya Tanzania ilidai kuwa inaidai Acaccia dola bilioni 190 abazo ni kodi kampuni hiyo ilikwepa kulipa toka ilipoanza shughuli zake nchini humo.
Japo Acacia ilakana, kampuni mama ya Barrick Gold ilikubali kufanya mazungumzo na serikali ya Tanzania na kufikia makubaliano ya kuanza upya kwa kuaminiana.
chanzo BBC
Comments
Post a Comment