Caf yasikia kilio cha Mourinho na Klopp
Kwa muda mrefu makocha wa ligi kubwa barani Ulaya wamekuwa wakulalamikia utaratibu wa chama cha soka Afrika CAf kufanya mashindano ya mataifa ya Afrika Afcon wakati ligi zikiwa zinaendelea.
Hii imekuwa ikizigharimu sana klabu za barani Ulaya kwa kuwakosa wachezaji wao muhimu wa Kiafrika wakati ligi ikiwa inaendelea lakini sasa shirikisho la mpira wa miguu Afrika Caf limesikia kilio cha vilabu hivyo.
Caf wameamua kuanzia sasa michuano hiyo mikubwa Afrika itakuwa ikifanyika mwezi June hadi July tofauti na mwanzo ambapo michuano hiyo ilikuwa ikifanyika kuanzia mwezi January hadi February.
Kuanzia mwaka 2019 ambapo mashindano hayo yatachezwa nchini Cameroon ratiba itabadilika huku timu zitakzoshiriki michuano hiyo nazo zikiongezeka kutoka timu 16 kama ilivyokuwa mwanzo hadi timu 24.
Makocha wa vilabu vya Uingereza akiwemo Jose Mourinho na Jurgen Klopp walikuwa wahanga wakubwa wa michuano ya Afcon lakini sasa watakuwa wamesaidiwa kwa kiasi kikubwa kubaki na wachezaji wao.
Ratiba nyingine ikiwemo ile mashindano kufanyika kila baada ya miaka miwili imebaki paleplae huku wazo la kualika baadhi ya timu kutoka katika mabara mengine likifutwa na sasa timu zitakazoshiriki zinabaki vile vile kuwa za kutoka bara la Afrika.
Comments
Post a Comment