Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli,aliwasili jana tarehe 3 Julai, 2017 amewasili mkoani Mwanza kwa ziara ya kikazi ya siku mbili na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongela
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli,aliwasili jana tarehe 3 Julai, 2017 amewasili mkoani Mwanza kwa ziara ya kikazi ya siku mbili na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongela pamoja na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Mwanza.
Akiwa mkoani hapa Mhe. Rais Magufuli atakuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa mradi wa uboreshaji wa huduma ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Sengerema leo tarehe 4 Julai, 2017.
Katika Uwanja wa Ndege wa Mwanza Mhe. Rais Dkt. Magufuli alikutana na kamati ya amani ya viongozi wa dini na kuwashukuru viongozi hao kwa sala na dua zao na amewataka waendelee kuwahimiza waumini wao kuliombea Taifa ili liepukane na vitendo vya rushwa ambavyo ni adui wa maendeleo.
Akiwa njiani kutoka Uwanja wa Ndege wa Mwanza katika eneo la Bwiru kuelekea Ikulu ndogo ya Mwanza, Mhe. Rais Magufuli msafara wake ulisimamishwa mara kwa mara na wananchi waliojaa barabarani na kuamua kuzungumza nao ambapo aliwahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imepania kupambana na ufisadi kwa lengo la kuwaletea maendeleo Watanzania bila kujali tofauti za dini au Siasa.
Aidha, aliwahakikishia wananchi hao kuwa Serikali yake imedhamiria kuondoa kero mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufuta baadhi ya kodi zenye kero na kuwapatia vitambulisho wafanyabishara wadogo wadogo, maarufu kama Wamachinga, ili waweze kufanya biashara zao bila kusumbuliwa.
Akiwa eneo la Nyamagana jijini Mwanza, Mheshimiwa Rais alitembea kwa miguu huku kuwasalimu wananchi waliokuwa wakimshangilia na kuzuia msafara wake.
Rais Magufuli pia alikwenda Uwanja wa Mpira wa Nyamagana na kuungana na baadhi ya wananchi waliokuwa wakiangalia mechi ya mpira wa miguu kati ya timu ya Buhongwe na Nyamwaga.
Mhe. Rais Dkt. Magufuli pia amefurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa barabara ya kutoka Uwanja wa Ndege wa Mwanza hadi katikakati ya jiji ambao gharama za ujenzi wake zilitokana na fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya sherehe za Muungano.
Comments
Post a Comment