Kivuli cha Bocco kinaendela kuwatesa Azam
Watu wengi bado hawaamini kama John Bocco ‘Adebayor’ kaondoka kwenye kikosi cha Azam, mmoja kati ya watu ambao wamesikitishwa na namna ambavyo nahodha huyo ameondoka katika timu hiyo ni shabiki mkubwa wa Azam anaefahamika kwa jina la Issa Azam ‘mjukuu wa Bakhresa.
Shabiki huyo amesema, kuondoka ni jambo la kawaida ila tatizo ni namna ambavyo Bocco ameondoka ambapo hata yeye hakuridhishwa.
“Suala la kuondoka kwa Bocco sio baya kwa sababu wenye timu wameamua kufanya mabadiliko na nia ya Azam ni kufika mbali.”
“Kuondoka Bocco kwa style ile hata mimi sijaelewa, mimi ninawaomba radhi mashabiki wa Azam Tanzania nzima kwa niaba ya Azam na uongozi. Watusamehe kwa sababu Bocco hatukumuondoa ipasavyo na kwa sababu sisi ni binadamu watusamehe.”
“Tunajua umuhimu wa Bocco na tunajua alikuwa anatusaidiaje na alipoitoa timu. Ni mchezaji mwenye nidhamu Tanzania nzima ana historia ya kuzifunga Simba na Yanga kila siku lakini mwisho wa siku historia yake imeishia pale tunamuomba na yeye atusamehe.”
“Kwa maoni yangu, Bocco angeandaliwa mechi ya kuagwa halafu sisi ambao tunampenda tungetoa zawadi zetu za heshima kwake kama ishara ya kumuaga, lakini ameondoka kimyakimya mimi sijafurahi. Juzi alinipigia simu tukaongea lakini hatukuongea mambo yanayohusu timu, naona aibu kwa sababu nipo ndani ya Azam.”
“Tunajipanga na timu mpya, asikwambie mtu Azam imekufa atakuwa anaongea uongo kwa sababu timu inakuja upya na malengo ni timu kuwa ya kutisha sana.”


Comments
Post a Comment